Ufafanuzi
Amesema Muadhi radhi za Allah ziwe juu yake: Tulikuwa pamoja na Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika safari, siku moja nikawa karibu naye tukiwa tunatembea, nikasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nieleze amali itakayoniingiza Peponi na kuniweka mbali na moto, akasema: Bila shaka umeuliza kuhusu jambo kubwa kulifanya kwake katika nafsi, na bila shaka ni jepesi na ni rahisi mno kwa atakayerahisishiwa na Mwenyezi Mungu kulifanya; tekeleza faradhi za Uislamu;
Ya kwanza: Umuabudu Mwenyezi Mungu peke yake na wala usimshirikishe na chochote.
Ya pili: Usimamishe swala tano za faradhi mchana na usiku: Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, Ishaa, kwa sharti zake na nguzo zake na wajibu wake.
Ya tatu: Utoe zaka ya wajibu, nayo ni ibada ya mali ya wajibu kwa kila mali iliyofikia kiwango katika sheria, na wanapewa wastahiki wake.
Ya nne: Ufunge mwezi wa Ramadhani, nako ni kujizuia na kula na kunywa na mengineyo katika mambo yenye kufunguza kwa nia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu, kuanzia kuchomoza kwa Alfajiri mpaka kuzama kwa Jua.
Ya tano: Utaizuru nyumba kwa kwenda Makka ili kutimiza ibada, kwa lengo la kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kisha akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Je nikufahamishe kuhusu njia inayokufikisha katika milango ya heri? Nayo ni kwa kutekeleza faradhi na sunna hizo:
Ya kwanza: Ni funga ya hiyari, nayo inamzuia mtu kuingia katika maasi, nayo ni kwa kuvunjavunja matamanio, na kuzidhoofisha nguvu.
Ya pili: Sadaka ya kujitolea inazima madhambi baada ya kuyafanya na huyaondosha na kufuta athari zake.
Ya tatu: Swala ya tahajudi katika theluthi ya mwisho ya usiku, kisha akasoma rehema na amani ziwe juu yake kauli yake Mtukufu: "Hunyanyuka mbavu zao" Yaani: Hujiweka mbali, na "malazi" Yaani: Mahali pa kulala, "wakimuomba Mola wao Mlezi" Yaani: kwa swala na dhikri na kusoma Qur'ani na dua, "kwa hofu na tamaa, na katika yale tuliyowaruzuku wanatoa, hakuna nafsi ijuayo yale waliyofichiwa, katika yale yenye kutuliza macho" Yaani: Yale yenye kutuliza macho yao siku ya Kiyama na katika pepo miongoni mwa neema, "ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyafanya".
Kisha akasema rehema na amani ziwe juu yake: Hivi nikueleze msingi wa dini? na nguzo yake inayosimamia? na kiini cha kilele chake?
Akasema Muadhi radhi za Allah ziwe juu yake: Ndio, nieleze ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu.
Akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Kichwa cha mambo yote ni: Uislamu nao ni shahada mbili, na kwa shahada hizi mbili ndio mtu anapata msingi wa dini. Na nguzo yake: Ni swala, hakuna Uislamu bila swala, kama ambavyo nyumba haiwezi kusimama pasina nguzo, atakaye swali dini yake itakuwa na nguvu na itanyanyuka; Na kiini cha kilele chake na kimo chake ni Jihadi na kutoa juhudi katika kupambana na maadui wa dini ili kulinyanyua neno la Mwenyezi Mungu.
Kisha akasema rehema na amani ziwe juu yake: Hivi nikuelezeni umadhubuti na ufanisi wa yaliyopita? Mtume rehema na amani ziwe juu yake akashika ulimi, na akasema: Zuia huu na wala usizungumze yale yasiyokuhusu. Akasema Muadhi: Je atatuchukulia makosa na kutuhesabu Mola wetu Mlezi na kutuadhibu kwa kila tunachozungumza?!
Akasema rehema na amani ziwe juu yake: Amekupoteza mama yako! Na makusudio yake si kumuombea dua mbaya, bali ni katika maneno ya waarabu yaliyokuwa yakitumika kumtanabahisha mtu kuwa jambo hili unatakiwa kulichukulia tahadhari kubwa na kulielewa, kisha akasema; na unadhani ni kipi kitawatupa watu na kuwadondosha kwa nyuso zao ndani ya moto zaidi ya chumo za ndimi zao, ikiwemo ukafiri na kumzulia mtu machafu na matusi na utesi na usengenyaji, na uongo na mfano wa hayo.