Ufafanuzi
Anaeleza Omari bin Khattwab -Radhi za Allah ziwe juu yake- kuwa Jibrili -Amani iwe juu yake- alijitokeza kwa Masahaba -Radhi za Allah ziwe juu yao- kwa sura ya mtu asiyejulikana, na miongoni mwa sifa zake nikuwa, nguo zake ni nyeupe mno, na nywele zake ni nyeusi mno, haonekani kuwa na athari za safari ikiwemo kuonyesha uchovu, vumbi, na nywele kutimka, na nguo kuchafuka, na hakuna yeyote amjuaye katika wote waliopo, nao wakiwa wamekaa kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-, akakaa mbele ya Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- mkao wa mwanafunzi, akamuuliza kuhusu Uislamu, akamjibu kwa nguzo hizi ambazo zimeambatana na kukiri shahada mbili, na kudumu na sala tano, na kutimiza zaka kwa wastahiki wake, na kufunga mwezi wa Ramadhani, na kutekeleza faradhi ya Hija kwa mwenye uwezo.
Muulizaji akasema: Sadakta!, Masahaba wakashangaa kwa swali lake la kuonyesha kuwa hajui kitu kwa muonekano wake, kisha anamsadikisha!.
Kisha akamuuliza kuhusu imani, akamjibu kwa nguzo hizi sita zilizokusanya kuamini uwepo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na sifa zake, na kumpwekesha kwa vitendo vyake kama kuumba, na kumpwekesha kwa ibada, nakuwa Malaika aliowaumba Allah kwa nuru ni waja waliotukuzwa hawamuasi Mwenyezi Mungu Mtukufu, na amri yake ndio wanayoifanyia kazi, na kuamini vitabu vilivyoteremshwa kwa Mitume kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama Qur'ani na Taurati na Injili na vinginevyo, na kuwaamini Mitume wenye kumfikishia Mwenyezi Mungu dini yake, miongoni mwao ni Nuhu na Ibrahim, na Mussa, na Issa, na wa mwisho wao ni Muhammadi -Rehema na amani ziwe juu yao wote- na wengineo katika Manabii na Mitume, na kuamini siku ya mwisho, na yanaingia hapa maisha baada ya kifo ikiwemo kaburi na maisha ya barzakh (Akhera), na kuamini kuwa Mwenyezi Mungu amekadiria mambo kulingana na ujuzi wake uliotangulia na hekima zake zikapelekea hivyo, na kuyaandika kwake, na matashi yake kwa mambo hayo, na kutokea kwake kwa namna aliyoikadiria Mwenyezi Mungu, na kuviumba kwake. Kisha akamuuliza kuhusu Ihisani, akamueleza kuwa Ihisani ni amuabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba anamuona, ikiwa hatoweza kufikia daraja hili basi amuabudu Allah kana kwamba Allah anamshuhudia, daraja bora zaidi kushuhudiwa, na ndio ya juu zaidi, na ya pili ni daraja ya kuchunga (Kuleta hisia kua unamuona mbele yako).
Kisha akamuuliza Kiyama ni lini? Akabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa elimu ya Kiyama ni katika elimu alizobaki nazo Mwenyezi Mungu ujuzi wake, hawezi kuijua yeyote katika viumbe, si muulizaji wala muulizwaji.
Kisha akamuuliza kuhusu alama za Kiyama? Akabainisha kuwa miongoni mwa alama zake ni kukithiri kwa wajakazi (Masuria) na watoto wao, au ni wingi wa watoto kutowatii mama zao, kiasi cha kuishi nao kama watumwa wao, nakuwa wachunga mbuzi na masikini watakunjuliwa dunia katika zama za mwisho, na watafaharishana katika kuremba majengo na kuyarefusha.
Kisha akaeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa muulizaji ni Jibril alikuja kuwafundisha Masahaba dini tukufu.